NAIROBI.
Tume ya Taifa ya uchaguzi nchini Kenya IEBC
inaendelea kupokea matokeo ya kura zilizokwisha pigwa ili kuzijumlisha kuweza
kupata matokeo ya jumla ya kura zote zilizopigwa wakati wa upigaji kura
uliofanyika siku tatu zilizopita nchini humo.
Wakati tume hiyo ikiendelea kupokea matokeo hayo,
muungano wa upinzani nchini humo umeendelea kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais
yanayoendelea kutangazwa na tume hiyo kwenye mtandao wake.
Viongozi wa muungano wa National Super Alliance
wamesema walikutana na wakuu wa Tume ya Uchaguzi Kenya ili kuwasilisha rasmi
malalamiko yao kupitia barua, wakati huohuo wakala mkuu wa upinzani Musalia
Mudavadi, ambaye ni naibu waziri mkuu wa zamani, amesema upinzani umepata
maelezo zaidi kwamba matokeo ya uchaguzi yalivurugwa baada ya kudukuliwa kwa
mitambo ya IEBC.
Wakuu wa IEBC wamekanusha kwamba mitambo
ilidukuliwa, mwenyekiti Wafula Chebukati amesema kulikuwepo na jaribio la
kudukua mitambo hiyo, lakini halikufanikiwa lakini Bw. Mudavadi amedai mgombea
wa upinzani Raila Odinga ndiye aliyeshinda uchaguzi huo.
“Twamtaka
mwenyekiti wa IEBC atangaze matokeo na kumtangaza Odinga na Kalonzo kama rais
mteule na naibu rais mteule wa Kenya mara moja,” amesema Bw Mudavadi.
Kwenye sheria
za nchi hiyo ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote kutangaza matokeo au
kusambaza matokeo ambayo hayajatoka kwa tume ya taifa ya uchaguzi, mwenye haki
ya kusambaza taarifa za uchaguzi ni tume hiyo ya uchaguzi pekee inayoruhusiwa
kutangaza matokeo.
PHOTO:
Sehemu ya soko kuu mjini Garissa, kaskazini mashariki mwa Kenya, imeteketea
baada ya mfarakano kati ya wafuasi wa wagombea wawili wa ugavana katika kaunti
hiyo.
Source: BBC
Post a Comment