0
Uchunguzi umeonesha kwamba kemikali aina ya Fipronil, ambayo inaweza kudhuru figo, ini na tezi za shingoni za mwanadamu, imekuwemo kwenye baadhi ya mayai yaliyokuwa yakiuzwa kwenye madukani.


Maofisa wakuu wa Afya wamekiri kuwa, mnamo mwezi Juni, walifahamu mayai kutoka Uholanzi, huenda yalikuwa yameharibiwa na dawa ya kuuwa wadudu, kashfa hii sasa imeigawa Ulaya na wasiwasi umeendelea kushuhudiwa katika nchi mbalimbali barani humo.
Tani za mayai zilikamatwa katika nchi kadhaa za Ulaya, wakati ambapo watu kadhaa walikamatwa na kumekua kukifanyika operesheni ya kusaka mayai hayo tangu siku ya Alhamisi nchini Uholanzi na Ubelgiji.
Siku ya Alhamisi (jana) jioni, Denmark ilitangaza kuwa tani ishirini za mayai yenye kemikali aina ya Fipronil yalikwishauzwa nchini humo, vilevile mashamba 180 ya kufugia kuku nchini Uholanzi yamefungwa kwa muda siku za karibuni huku uchunguzi ukiendelea.
Uchunguzi kuhusu udanganyifu unaosababishwa na kuharibika kwa mamilioni ya mayai barani Ulaya kutokana na kemikali aina ya Fipronil, dawa inayotumiwa kwa kuua viroboto na kupe kwenye kuku, ya kampuni kubwa Ujerumani ya BASF inaendelea kuzua hali ya sintofahamu barani ulaya.
Hayo yakijiri, maduka ya jumla barani Ulaya yamesitisha uuzaji wa mayai kutoka kwa vifurushi vya mayai ambavyo huenda viliambukizwa sumu hiyo, hata hivyo, Aldi, ambao wana karibu maduka 4,000 nchini Ujerumani, ndio wa kwanza kusitisha uuzaji wa mayai kama tahadhari.
Uholanzi ndiyo muuzaji nje mkubwa zaidi wa mayai na bidhaa za mayai Ulaya, na miongoni mwa muuzaji mkubwa duniani na inakadiriwa kwamba taifa hilo huzalisha zaidi ya mayai bilioni 10 kila mwaka, na asilimia 65 kati ya hayo huuzwa nje ya nchi hiyo.


Source: RFI

Post a Comment

 
Top