0
PHOTO: IGP Simon Sirro
PWANI
Mara baada ya kuapishwa na kuwa Mkuu wa jeshi la polisi nchini, wananchi wa wilaya za Kibiti na eneo la Mkuranga Mkoa wa Pwani wamesema iwapo mkakati wa Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro ni kukomesha mauaji aanze kwa mazungumzo na wananchi hao. 
Wamesema kuwa kwa kufanya mazungumzo na wananchi atabaini sababu zilizopelekea mauaji hayo na wahusika wanaoendesha mauaji hayo pia kupata suluhisho lake.
Mkazi mmoja wa Kibiti aliyejitambulisha kwa jina la Alhaji Msumi alisema IGP Sirro anapaswa kufika kwenye wikaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga kisha kufanya mazungumzo na wazee katika vijiji vya Bungu, Kibiti na Ikwiriri.
Mzee mwingine wa Ikwiriri ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema uzoefu wa Sirro katika utulizaji na utatuzi wa matatizo utafanikisha kuwabaini watu au kikundi wanaoendesha mauaji katika wilaya hizo.
“Tunafahamu uzoefu alionao IGP Sirro, hivyo tunaimani suala la mauaji atalikomesha mara moja,” alisema.
Mwananchi huyo ameongeza kuwa kwa muda mrefu polisi walikuwa wakijua wilaya hizo hazipo salama kutokana na kukumbwa na matukio ya mauaji mara kwa mara, lakini walikuwa wazito kuanza kuusaka mtandao huo.
Amesema harakati za kuwasaka watu hao zimeanza pale yalipotokea mauaji ya aliyekuwa Ofisa Upelelezi Wilaya ya Kibiti, Peter Kubezya na wengine wawili ndipo walipoanza kuchukua hatua huku wakiwa wamechelewa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Gullamuhussein Kifu amesema hali ya usalama inazidi kuimarika siku baada ya siku na kuwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuwakamata watuhumiwa wote.


Source: Mwananchi

Post a Comment

 
Top