WANAWAKE
wanne katika Kijiji cha Kihumbu, Kata ya Hunyari wilayani Bunda,
wamejeruhiwa kwa kupigwa na vitu vizito, zikiwamo fimbo, rungu, bapa za panga
na katani, baada ya kutuhumiwa kumuua kwa uchawi, mwanafunzi Waryo Mseti
(12).
Tukio
hilo lilitokea juzi mchana katika kijiji hicho wakati mwili wa mwanafunzi huyo
aliyekuwa akisoma darasa la nne katika Shule ya Msingi Kihumbu ukisubiri
kuzikwa.
Ilidaiwa
kuwa baada ya Mseti kufariki dunia, wazazi wake kwa kushirikiana na Mwenyekiti
wa Kitongoji hicho, Hasha Hamisi, walikwenda kupiga ramli kwa mganga wa
kienyeji wakidai mtoto huyo alikufa kifo cha ushirikina.
Ofisa
Mtendaji wa Kijiji hicho, Chacha Warioba, alidai mganga huyo baada ya kufanya
dawa zake, alieleza kuwa mwanafunzi huyo alikuwa amechukuliwa kichawi na
wanawake hao na alikuwa bado yuko hai ila walikuwa wamemficha sehemu.
“Nathibitisha
ni kweli tukio hilo lipo, polisi walifika hapa kijijini na kuwachukuwa wanawake
hao na kuwapeleka Kituo cha Polisi Bunda. Wakati tukio hilo linatokea mimi
sikuwapo hapa kijijini,” alisema Warioba.
Inadaiwa
kuwa Hamisi aliyewapeleka wazazi wa mwanafunzi huyo kwa mganga, aliwaeleza
wenzake kuwa hata yeye aliwaona wachawi hao kwenye kioo cha maji ya mganga wa
jadi. kauli hiyo ilithibitishwa kwa waombolezaji waliokuwapo nyumbani hapo
wakati maiti ya mtoto huyo ikiwa ndani ikisubiri kuzikwa.
Baada ya
kuelezwa hayo, baadhi ya waombolezaji walianza kuwasaka wanawake
hao wanaotuhumiwa kwa uchawi.
Waliwakamata mmoja baada ya mwingine
na kuwapeleka mlimani, huku wakiwa wamewafunga kamba na wakiwatishia
kuwachinja, Waliwapiga na kuwataka wamrudishe mtoto huyo
Wanawake
hao (majina tunayo), wote wakazi wa Kijiji cha Kihumbu, walisema
walifanyiwa unyama na ukatili huo unaohusisha imani za ushirikina, na hata
nyumba ya mmoja wao ilimwagiwa mafuta iweze kuteketezwa kwa moto.
“Walitupiga
sana kwa fimbo, mabapa ya mapanga, rungu na katani, walituteka hadi milimani
wakitulazimisha tumrudishe huyo mtoto waliodai tumemuua, mimi walinilaza chini
na wakaniwekea panga shingoni, eti wanichinje kama sitaki kusema ukweli, Lakini
nilikataa kwamba sijui chochote.” alisema mmoja wa wanawake hao.
Wanawake
hao waliokolewa na polisi waliofika katika eneo la tukio na kuwachukua hadi
Kituo Kikuu cha Polisi Bunda kabla yakuwapeleka katika Hospitali Teule ya
Wilaya ya Bunda (DDH). Bado wamelazwa hospitalini hapo baada ya kujeruhiwa
katika tukio hilo na muuguzi wa zamu katika Wodi ya Wanawake, Daria John,
alisema hali zao zinaendelea vizuri.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhani Ng’anzi, alisema wote waliohusika
kujichukulia sheria mkononi lazima wakamatwe na kufikishwa mahakamani.
Post a Comment