Shirika lisilokuwa la kiserikali la Plan International wameishauri Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi nchini (VETA) kuongeza walimu waliobobea katika ufundishaji wa wanafunzi walemavu ili kuhakikisha wanapata elimu sawa na wengine.
Ushauri huo umetolewa na Meneja wa Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) - Tanzania, Simon Ndembeka baada ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaohitaji kupatiwa elimu ya ufundi katika vyuo hivyo.
PICHA: Meneja wa Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) - Tanzania, Simon Ndembeka akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu uhitaji wa walimu wa mahitaji maaalum watakaoweza kukidhi idadi ya wanafunzi walemavu wanaohitaji kupatiwa elimu ya ufundi katika Chuo cha Elimu na Ufundi Stadi (VETA) chini ya mradi huo.
Meneja Mradi amesema kuwa nyakati za kuwaficha walemavu majumbani zimekwisha na kwa sasa wazazi wanafahamu kuwa ulemavu sio mwisho wa maisha hivyo muamko wa walemavu wanaohitaji kusoma umekuwa mkubwa tofauti na zamani.
“Mradi huu umetenga asilimia 10 kwa ajili ya jamii ya vijana wenye ulemavu kupatiwa mafunzo ya ufundi katika chuo cha VETA ili baadae waweze kuendesha maisha yao lakini lengo hilo lina changamoto kubwa ya upungufu wa walimu wa taaluma hiyo hivyo, tunaishauri VETA kuongeza walimu wa aina hiyo ili kukidhi uhitaji wa idadi ya wanafunzi walemavu”, alisema Ndembeka.
Ndembeka ameongeza kuwa kitendo cha kuwawezesha vijana wenye ulemavu ni moja ya lengo la mradi huo kwani kundi hilo ndilo kundi lenye changamoto nyingi za kimaisha kuliko kundi lingine lolote hivyo kuwapatia elimu kutawasaidia kuweza kupata ajira au kujiajiri na hatimaye kuweza kuyakomboa maisha yao.
PICHA:Baadhi ya Vijana waliohitimu katika fani ya ufundi wa magari chini ya Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) wakifanya mazoezi ya kurekebisha magari katika gereji ya Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, (mwenye tisheti jekundu) ni fundi msaidizi wa gereji hiyo, Haji Faki.
Aidha, Ndembeka ameishukuru Serikali kwa ushirikiano wao wa kutoa misaada ya mikopo, elimu, maeneo ya vijana kufanyia mazoezi pamoja na ushiriki wao kama wageni rasmi katika mahafali mbalimbali za vijana wanaohitimu elimu ya ufundi chini ya mradi huo.
Kuhusu suala la kuwasaidia vijana kupata ajira amefafanua kuwa mara nyingi wamekuwa wakifanya vikao na waajiri wa sekta mbalimbali nchini ili kuwajengea ufahamu waajiri juu ya uwepo wa vijana hao pamoja na kujadili jinsi ya kuwasaidia kwa kuwapatia ajira.
Mradi huo wa miaka mitatu unatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya VSO, CCBRT, VETA, UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku ukiratibiwa na Shirika la Plan International chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).
Post a Comment