0
KAMATI ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) imekifungulia rasmi kituo cha radio Magic fm cha jijini Dar es Salaam wakati huo huo kituo cha Radio five cha jijini Arusha, kikifungiwa kwa miezi mitatu na kutakiwa kulipa faini/adhabu ya sh. milioni tano, pamoja na kuwa chini ya uangalizi kwa mwaka mmoja.

Akizungumza  jijini Dar es Salaam makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Joseph Mapunda alisema kuwa uamuzi huo umetokana baada ya kamati hiyo kukaa kwa pamoja na viongozi wa pande mbili na kuwasikiliza na kutafakari kwa kina maelezo ya utetezi yaliyotolewa na viongozi hao.

Mapunda alisema kwa mujibu wa kamati hiyo kituo cha Magic fm kinadaiwa kukiuka kanuni za maudhui kupitia kipindi chake cha Morning Magic kipengele cha Paka Rangi ambacho kilirushwa hewani kati ya saa 1.00 asubuhi na 2.00 asubuhi.

Alisema watangazaji wa kipindi hicho wanadaiwa kutoa maudhui yenye kebehi yaliyolenga kumdharirisha Rais, Taasisi ya Rais na kusababisha uvunjifu wa amani na kuhatarisha usalama wa taifa, hivyo kituo hicho kimepewa onyo kali pamoja na kutakiwa kuomba radhi kwa muda wa siku tatu mfululizo.

“Baada ya kusikiliza na kutafakari kwa kina maelezo ya utetezi yaliyotolewa na Uongozi wa Magic fm radio, Kamati ya Maudhui imeridhika kuwa kipindi cha Morning Magic kilikiuka baadhi ya kanuni za 2005 za huduma za utangazaji na  Kamati hiyo inaamua kutoa onyo kali kwa Magic Radio”, alisema.

Pamoja na  kumuomba radhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh John Pombe Magufuli, wasikilizaji, wananchi kwa ujumla, pamoja na Tangazo la kuomba radhi litolewe kwa siku tatu mfululizo katika taarifa za habari za saa 10.00 alasiri,  3.00 usiku kuanzia kesho (leo).

Mapunda aliongeza kuwa kwa upande wa kituo cha Radio Five cha Arusha ambacho kilirusha maneno yaliyo tamkwa na Mbunge wa Jimbo la Arusha mjini Godbless Lema ikiwemo maneno ya kashfa yaliyolenga kumdhalilisha Rais John Magufuli na Serikali kwa ujumla.

Pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki katika maandamano ya UKUTA yaliyopigwa marufuku na Jeshi la Polisi,
“Maneno ya Lema yalilenga kuhamasisha wananchi kupambana na jeshi la polisi na hivyo kusababisha uvunjifu wa amani na kuhatarisha usalama wa Taifa,” alisema.

Mapunda aliongeza kuwa  uamuzi huo umetolewa na kamati hiyo baada ya kusikiliza maelezo ya utetezi yaliyotolewa na wa Uongozi wa Redio 5.

Alibainisha kuwa baada ya kusikiliza maelezo ya utetezi kamati imeridhia kuwa kipindi cha matukio kilikiuka baadhi ya kanuni za maudhui namba 5(a,b,c,d,f,h) 6(2) (b, c) na 18 (1) (b).

Alifafanua baada ya kuridhia na utetezi uliolewa na viongozi wa  kituo hicho, kwa mujibu wa kamati ya maudhui kituo  kinatozwa faini ya sh. Milioni 5 ambazo zitatakiwa kulipwa ndani ya siku 30 kuanzia jana , kinafungiwa kwa miezi 3 na kuwekwa chini ya uangalizi maalumu kwa muda wa Mwaka 1 baada ya kipindi cha kufungiwa kumalizika.

Mapunda alisema mbali na uamuzi huo wahusika wana haki ya  kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo  iko wazi ndani ya siku 30 kuanzia jana. Uamuzi huo umesainiwa na Makamu Mwenyekiti Joseph Mapunda pamoja na wajumbe wa kamati ya maudhui Abdul Ramadhan Ngarawa pamoja na Derek Kaitira Murusiri.

Radio hizo zilifungiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni na Sanaa na Michezo, Nape Nnauye Agasti 29 mwaka huu.

Post a Comment

 
Top