0
Shirika la Plan International limetoa rai kwa vijana wanaoishi katika mazingira magumu kuchangamkia fursa za elimu ya ufundi zinazotolewa na Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA) chini ya mradi wa uwezeshaji vijana kiuchumi (YEE) unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya.

Rai hiyo imetolewa leo na Meneja wa shirika hilo wa Halmashauri ya Kibaha Bw. Emmanuel Mmbaga alipokuwa akizungumzia mikakati, malengo, nia na madhumuni ya kuanzisha mradi huo wa vijana ambao unaratibiwa na shirika hilo.

Mmbaga amesema kuwa mradi huo una lengo la kuwasaidia vijana kupata elimu ya ufundi katika fani mbalimbali ambapo nia na madhumuni ikiwa ni kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kuendesha maisha yao ili kupunguza kasi ya umasikini nchini.

“Mradi huu umelenga vijana wanaoishi katika mazingira magumu ambao wanatamani kujiendeleza kielimu lakini hawana uwezo huo hivyo tunawasihi vijana mchangamkie fursa iliyotolewa kupitia shirika letu ili muweze kuendeleza maisha yenu”, alisema Mmbaga.

Meneja huyo ameongeza kuwa vijana wengi wamekuwa wakidharau fursa zinazotolewa na mashirika mbalimbali lakini amewasisitiza kuwa mradi huo ni wa uhakika na matunda ya vijana waliohitimu yameanza kuonekana kwani kuna baadhi wamebahatika kupata ajira serikalini na katika makampuni binafsi pia wengine wameweza kujiajiri wenyewe.

Naye Mkuu wa Chuo cha VETA - Pwani, Joseph Deusdedit amesema kuwa kadri mradi unavyoendelea ndivyo wavyozidi kutoa nafasi nyingi za vijana kupata elimu ya ufundi katika chuo hicho pia wameendelea kuwatengea sehemu za kupata mafunzo zilizo karibu na maeneo wanayoishi kwa ajili ya kuwawezesha kutambua kiurahisi fursa zilizopo katika maeneo yanayowazunguka pia kuwapunguzia gharama za usafiri.

“Baada ya kuona uhitaji wa elimu hii umekuwa mkubwa tumeona tuongeze idadi ya vijana kutoka vijana 602 waliohitimu awamu mbili zilizopita hadi kufikia vijana 813 ambao wanaendelea na masomo hivi sasa hivyo, tunawaomba vijana mjitokeze kwa wingi ili kupata mafunzo hayo”, alisema Deusdedit.

Ameahidi kushauriana na wadau wengine kufanya elimu hii ya vijana wanaoishi kwenye mazingira magumu kuwa endelevu hata kama mradi hautoendelea kwa sababu mradi huo umeonyesha mafanikio na unalenga vijana wa aina zote wakiwemo walemavu, waliosoma na wasiosoma hivyo kuondoa adha kubwa ya utegemezi katika familia zao.

Mradi huu wa miaka mitatu unafanyika katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam, unatekelezwa kwa ushirikiano wa shirika la VSO, UHIKI, CODERT, CCBRT pamoja na ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, vijana na watu wenye ulemavu.

Post a Comment

 
Top