0




HABARI KWA UNDANI: Serikali chini ya Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa siku 14 kwa Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili(MOI) Dkt. Othman Kiloloma kukaa na bodi ya taasisi hiyo kushughulikia matatizo ya watumishi ili kuleta ufanisi mzuri katika kitengo hiko.

Akizungumza na watumishi wa MOI Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amemtaka Dkt. Kiloloma kukaa na bodi ya taasisi hiyo ili kupata ufumbuzi wa matatizo ya watumishi wake ndani ya siku 14 ili wafanyakazi waweze kutoa huduma bora kwa watanzania.



“Naagiza Bodi ya MOI pamoja na Kaimu Mkurugenzi wake ili kupata ufumbuzi wa matatizo ya watumishi wake ndani ya siku 14 ili kuondoa malalamiko na kuleta ufanisi bora katika taasisi hii”alisisitiza Mhe. Ummy.


Aidha Mhe. Ummy amesema kuwa amepokea changamoto zao na za taasisi hyo nakuhaidi kuzitatua ndani ya mwezi mmoja na kuwataka wasichoke kutoa huduma bora kwa watanzania ili kuokoa maisha yao na kupambana na umaskini.

Mbali na hayo Mhe. Ummy ameagiza watendaji wa Wizara yake kuleta mkakati wa kupambana na kupunguza ajari za barabarani hasa zitokanazo na bodaboda ndani ya siku 14 ili kuwapa nafuu madaktari na wauguzi wa MOI kuweza kuondoa mlundikano wa wagonjwa hospitalini hapo.

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi  MOI Dkt.Othman Kiloloma amesema kuwa mbali na changamoto wanazokutana nazo wamefanikiwa kuunda upya wafanyakazi wataoweza kufanya upasuaji kwa wagonjwa wa jumamosi na itaanza mara moja.

Aidha Dkt. Kiloloma ameongeza kuwa MOI imeweza kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 1.1 kwa mwezi kutoka kiasi cha shilingi milioni 400 kwa kipindi kilichopita.

Na Mathias Chikoka

Post a Comment

 
Top