0



Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo,Freeman Mbowe  ametangaza kusitishwa kwa maandamano ya Oparesheni UKUTA yaliyokuwa yamepangwa kufanyika kesho September mosi nchi nzima.

Akizungumza na wanahabari leo, makao makuu ya chama hicho, Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Mbowe amesema, Chadema inalazimika kuahirisha maandamano na mikutano yote kwa siku ya kesho kutokana na kuheshimu wito wa viongozi wa dini zote waliowaomba.

“Viongozi wa dini zote hapa nchini kuanzia, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Mkuu wa Kanisa la Kianglikana Tanzania, Rais wa Baraza la Maaskofu (TEC), Katibu Mkuu wa Baraza la Kikristo Tanzania (CCT), Mkuu wa Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT), Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste (CPCT), Mufti Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) na Mufti Mkuu wa Zanzibar, wametusihi tuahirishe ili wao wazungumze na Rais John Magufuli kutafutia suluhu suala hili,”
amesema Mbowe.

Mbowe amezitaja taasisi na watu mbalimbali wenye heshima kubwa ndani na nje ya nchi waliokiomba chama hicho kuahirisha maandamano na mikutano hiyo kuwa ni Mzee Joseph Butiku ambaye ni Mwenyekiti wa Tasisi ya Mwalimu Nyerere, Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA),  Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) pamoja na mjane wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mama Maria Nyerere ambaye alizungumza na Edward Lowassa kwa niaba ya chama hicho.
 

Mh mbowe alisema, “Kwa heshima ya viongozi wetu wa dini na taasisi hizi, tunawatangazia wanachama wetu kote nchini kuwa tunaahirisha maandamano hayo kwa muda wa mwezi mmoja ili kuwapa nafasi viongozi hawa waonane na Rais Magufuli na kama asipowaelewa hata hao, sisi tusilaumiwe,”

Post a Comment

 
Top