DAR ES SALAAM.
Dereva na kondakta wa daladala
alilopanda mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina
Akwiline aliyeuawa juzi kwa kupigwa risasi na polisi wamesimulia mkasa
ulivyokuwa. kwilina alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa
Shahada ya Ununuzi na Ugavi (Procurement and Logistics) katika chuo hicho,
lakini maisha yake yalikatishwa juzi akiwa ndani ya basi la daladala.
PHOTO: Akwilina Akwiline wakati wa Uhai wake. |
Tukio hilo lilitokea wakati polisi wakiwatawanya wanachama
wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe waliokuwa
wakielekea katika ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kinondoni, Aaron
Kagurumjuli kudai hati za viapo vya mawakala wao.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alikiri kuwapo kwa kifo cha mtu mmoja
aliyepigwa risasi na askari wakati wakizuia maandamano hayo. Wakizungumza na
Mwananchi, kondakta na dereva wa daladala alilokuwa amepanda mwanafunzi huyo
akitokea katika chuo hicho eneo la Mabibo kwenda Makumbusho walisema alipigwa
risasi wakiwa Mkwajuni, Kinondoni baada ya kuwakuta wafuasi wa Chadema
wakiandamana.
Alisema alipokuwa akiingia kwenye gari mwanafunzi huyo alikuwa akiongea kwa simu na hakukaa kwa sababu hakukuwa na kiti kilichokuwa wazi, “Daladala iliendelea na safari kama kawaida, tulipakia na kushusha abiria. Tulipofika kituo cha Magomeni Kanisani abiria walikuwa wamepungua, hivyo yule dada alikwenda kukaa siti ya mwisho kabisa,”
Alisimulia kuwa wakiwa kwenye mteremko wa Mkwajuni, aliona
kundi la watu mbele yao huku kukiwa na magari ya askari lakini wao waliendelea
na safari. “Wakati
huo nilikuwa nimetoka nyuma kuchukua nauli, ile narudi kwenye mlango
nikashangaa kelele za abiria ile nageuka nijue kuna nini nikaona kitu kimepita
sikioni shaa! kumbe ilikuwa risasi”
“Kabla
sijafanya chochote wakati huo nashangaa dereva akaniambia lala chini
umeshaumia, ile nainama nikashangaa damu inamwagika kumbe risasi ilikuwa
imenipitia.”
Dereva wa daladala hilo, Shaaban Mohammed alisema aliposikia
milio ya risasi huku ndani ya basi abiria wakipiga kelele, aliamua kusimama ili
ajue kinachoendelea. Alisema kwa sababu nje kulikuwa na fujo, huku ndani ya
basi abiria mmoja akiwa ameanguka, ilibidi awaamrishe abiria wote walale chini
kuokoa uhai wao kwa kuwa alishaona risasi zinapigwa.
PHOTO: Kondakkta wa daladala alilokuwemo Akwilina akionyesha tundu la risasi. |
“Kondakta
wangu naye damu zilikuwa zinamwagika nikamwambia alale haraka, kwa hiyo wote
tulikuwa tumechanganyikiwa wakati huo,” alisema Mohammed, wakati hayo
yakitokea ilikuwa takriban saa 11:30 jioni.
“Gari
lilitapakaa damu na mwanafunzi aliyekuwa amepigwa risasi alikuwa ameanguka,
kila mtu akawa haelewi nini kifanyike,” alisema. Baada ya tukio hilo, dereva
huyo aliamua kuondoa basi katika eneo hilo na alipofika Kinondoni Studio
alimuona askari wa usalama barabarani (trafiki) na kumweleza kilichotokea
akimuomba msaada na hiyo ikiwa ni baada ya kubaini kuwa mwanafunzi huyo alikuwa
ameshafariki dunia.
Alisema alielekezwa kwenda kituo kidogo cha polisi kilicho
jirani na ukumbi wa Vijana CCM Kinondoni na baada ya kufika na kujieleza,
hawakuandikisha maelezo yoyote wala kupewa karatasi, bali waliongozana na
askari aliyekuwa amevalia kiraia hadi Hospitali ya Mwananyamala.
“Mwili
wa yule mwanafunzi ulishushwa,”
alisema Mohammed ambaye alieleza kuwa ni mgeni jijini Dar es Salaam alikofika
mwezi uliopita akitokea Tanga.
Kondakta Abdallah alisema alipatiwa
huduma ya kwanza na aliandikiwa dawa ambazo bado hajanunua kwa kukosa fedha. “Najihisi kichwa
kizito, kinauma na niliandikiwa dawa, hivyo namsubiri bosi wangu nipate fedha
za matibabu” alisema.
Dereva Mohammed alisema tangu tukio hilo la juzi
lililosababisha vioo vya gari kuvunjika wameliegesha basi hilo wakiamini
watafidiwa kwa uharibifu huo ili waendelee na kazi za kila siku.
Shuhuda mwingine
Shuhuda mwingine wa tukio hilo, Noel Shao ambaye alikuwapo
wakati mwili wa marehemu ukifikishwa Mwananyamala alisema, “Nilishiriki katika kuuhifadhi mwili wa
Akwilina. Alivalia suruali ya jeans iliyokuwa na takriban Sh25,300 tena noti za
elfu tano tano, ambazo alikabidhiwa ndugu yake baada ya kufika. Hakika lilikuwa
ni tukio la kusikitisha sana.”
Simulizi chuoni NIT
Baada ya taarifa za kifo cha mwanafunzi huyo kufika NIT,
vilio, huzuni na majonzi vilitawala. Hata jana mchana wakati waandishi wetu
walipofika chuoni hapo, waliwakuta wanafunzi wakiwa katika vikundi huku karibu
wote wakiwa na nyuso za huzuni.
Hata hivyo, licha ya kusema kwamba wamepata taarifa za tukio
hilo uongozi wa NIT kupitia kwa Ofisa Uhusiano, Ngasekela David ulisema suala
hilo lipo katika mikono ya polisi na familia yake.
“Tulipata
taarifa za msiba wa mwanafunzi huyu kutoka kwa mwanafunzi mwenzake aliyekuwa
anaishi naye nje ya chuo, tumesikitishwa na kifo chake hivyo tunaendelea
kuwasiliana na familia kujua utaratibu,” alisema. Rafiki wa mwanafunzi huyo,
Hidaya Shaaban alisema Akwilina alimuaga kuwa anaelekea Bagamoyo mkoani Pwani
kupeleka barua ya mafunzo kwa vitendo.
“Najisikia
vibaya na nimeumia, aliniaga anaenda kupeleka barua yake ya ‘field’ na alikuwa
nayo kweli, jioni nikashangaa kupata taarifa kuwa amepata ajali na sikujua
ajali gani lakini baadaye nikaambiwa mauti imemfika” alisema.
Alisema awali hakujua kama alifariki dunia kwa kupigwa
risasi. Paul Sabuni ambaye ni kiongozi wa darasa alilokuwa akisoma Akwilina,
alisema kabla ya kifo chake alifika chuoni kusaini ‘course work’.
“Alikuja
saa tisa kuangalia matokeo yake na kwa kweli alikuwa amefanya vizuri, alikuwa
msichana mzuri anayejituma darasani, tumeumia mno. Sikuwahi kusikia kama
anajihusisha kwa namna yoyote na siasa wala chama,” alisema
Sabuni ambaye ni waziri wa mikopo wa serikali ya wanafunzi wa NIT.
Ndugu
wa wamlilia: Tugolena Richard Uiso, ambaye ni
dada wa Akwilina akizungumza na Mwananchi alisema familia ilishtushwa na
taarifa za kifo chake.
Alisema awali hawakuamini kwa sababu walijua yupo chuoni. “Jana jioni
(juzi) tulipata taarifa amepigwa risasi Kinondoni na amepelekwa hospitalini
Mwananyamala, tulishangaa ikabidi twende kuhakikisha ile taarifa,”
alisema.
Alisema baada ya kwenda hospitalini waliutambua mwili na
kuthibitisha kuwa ndiye mtoto wao. “Leo asubuhi wenzetu wameamkia Polisi Oysterbay,
wameambiwa mwili utapelekwa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi, tumebaki na
simanzi tunasubiri kinachoendelea,” alisema.
Alisema Akwilina ni mtoto wa sita kwa wazazi wake wanaoishi
Olele wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro wakijishughulisha na kazi za kilimo na
ufugaji na alifika Dar es Salaam kwa ajili ya masomo.
Kauli za wadau
Kutokana na tukio hilo, Mtandao wa Watetezi wa Haki za
Binadamu katika taarifa kwa vyombo vya habari umesema umepokea kwa masikitiko
kifo cha mwanafunzi huyo.
“Mauaji
haya ya kikatili yanasikitisha sana na sisi kama watetezi wa haki za binadamu
tunalaani vikali vitendo hivyo kwa kuwa ni kinyume kabisa na haki za binadamu,” inasema
taarifa hiyo iliyosainiwa na mratibu wake Onesmo Olengurumwa.
“Tunaviomba
vyombo husika kuchukua hatua stahiki kwa waliotekeleza mauaji ya raia wasiokuwa
na hatia,” alisema.
Chama cha ACT Wazalendo kimesema kimepokea kwa masikitiko
tukio la mauaji ya mwanafunzi huyo.
“Tunasikitika
na tunakataa kuona Tanzania inaingia katika ubaguzi wa vyama. Utu na heshima ya
binadamu wa Tanzania hauwezi kupimwa na uvyama,” inasema taarifa hiyo iliyotolewa na mwenyekiti wake,
Yeremia Maganja akiwaomba viongozi wa dini na makundi mengine ya jamii kukemea
mauaji hayo.
Post a Comment