0
DAR ES SALAAM.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa taarifa ya kuzifutia leseni ya biashara kwa benki tano na kuziweka chini ya ufilisi kwa kipindi kijacho.

Katika taarifa iliyotolewa mapema leo na BoT imezitaja benki hizo kuwa ni Kagera Farmers' Cooperative Bank Limited, Covenant Bank For Women (Tanzania) Limited, Njombe Community Bank Limited, Efatha Bank Limited, na Meru Community Bank Limited.

Taarifa hiyo ya BoT imesema kuwa imefanya uhamuzi huo kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha 56(1)(g), 56(2) (a), (b) na (d), 58(2)(i), 11(3)(c) na (j), 61(1) na 41(a) cha sheria ya mabenki na taasisi za fedha ya mwaka 2006, Benki kuu ya Tanzania imeamua kuzifunga, kusitisha shughuli zake zote za kibenki, kufuta leseni zake za biashara ya kibenki pamoja na kuziweka chini ya ufilisi.

“Kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu Na. 41(a) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006; Benki Kuu ya Tanzania imeiteua Bodi ya Bima ya Amana (The DEPOSIT INSURANCE BOARD) kuwa mfiiisi kuanzia tarehe 04 Januari 2018,” ilisema taarifa hiyo.

PHOTO Profile: Efatha Bank Limited mojawapo ya benki mufilisi.

“Uamuzi huu umechukuliwa baada ya Benki Kuu ya Tanzania kujiridhisha kuwa benki hizi zina upungufu mkubwa wa mtaji kinyume na matakwa ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake. Upungufu huo wa mtaji unahatarisha usalama wa sekta ya fedha na kwamba kuendelea kutoa huduma za kibenki kwa benki hizo kunahatarisha usalama wa amana za wateja wake.”


Taarifa hiyo imeeleza kuwa BoT inapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta uhimilivu katika sekta ya fedha.

Post a Comment

 
Top