0

DAR ES SALAAM.
Wasanii wa muziki wa kizazi kipya, Hamisi Mwinyijuma na Ambwene Yesaya wameendelea ‘kuigaragaza’ mahakamani kampuni huduma za simu za mkononi ya Tigo, baada ya Mahakama ya Wilaya ya Ilala kutupilia mbali maombi yake.
Kampuni hiyo ilikuwa ikiiomba mahakama hiyo iamuru kampuni ya Cellulant Tanzania Limited, ijumuishwe kwenye hukumu hiyo, kama mmoja wa wadaiwa, kwenye hukumu ya Mahakama hiyo iliyoiamuru kuwalipa wasanii hao fidia ya Sh2.1 bilioni.
Hata hivyo leo Jumatano mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi hayo baada ya kukubaliana na hoja za wasanii hao kupitia kwa wakili wao, Albert Msando kuwa utaratibu walioutumia kutoa maombi hao sio sahihi.
Katika maombi hayo, Tigo walikuwa wakiomba mahakama hiyo iamuru kampuni hiyo ijumuishwe kwenye hukumu hiyo chini ya kifungu cha 96 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai, wakidai kuwa kampuni hiyo pia ina hoja za kujibu.
Tigo ilikuwa inadai kuwa Cellulant ndio iliyowapelekea nyimbo hizo na kwamba yenyewe haikujua kama kampuni hiyo haikuwa na makubaliano na wasanii hao.
Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, wasanii hao kupitia kwa wakili wao walipinga madai hayo wakidai kuwa kifungu walichokitumia hakitoi mamlaka kwa Mahakama kumuongeza mdaiwa mwengine kwenye kesi ambaye hakuwepoa awali.
Akitoa uamuzi huo leo Jumatano, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ritha Tarimo alikubaliana na hoja za wakili wa wasanii hao akisema kuwa kifungu kilichotumika kufungua maombi hayo hakihusiki na nafuu walizokuwa wanaziomba.

Source: Mwananchi.

Post a Comment

 
Top