0
PROFILE PHOTO: 'Nay wa Mitego'
DODOMA.
Waziri wa Habari, utamaduni, sanaa na michezo, Dkt Harrison Mwakyembe ameliomba jeshi la polisi kumuachia msanii wa Bongofleva Emmanuel Elibariki maarufu kama “Nay wa Mitego” aliyekuwa anashikiliwa kwa tuhuma za kutoa wimbo usio na maadili uliojulikana kama “WAPO”.
Akizungumza mjini Dodoma, Mwakyembe amesema kuwa aliwasiliana na Rais ambaye alimuelekeza kuwa wimbo huo haukuwa na shida yoyote ya kimaadili na kwamba hata yeye binafsi ameupenda na anamtaka msanii huyo aongeze baadhi ya mabeti kwenye wimbo wake.
“Kwakweli ule wimbo ni mzuri hata mheshimiwa Rais amesema anaupenda na kusema ukweli ile biti imetulia,” amesema waziri Mwakyembe wakati akitoa ufafanuzi kuhusiana na wimbo huo.
Waziri Mwakyembe amesema kuwa Rais Magufuli amependekeza kwenye wimbo wake aongeze kama maneno “hata wakwepa kodi...wapoo”! Ili kuufanya unoge zaidi kutokana na ujumbe wake kuwa ulilenga kuiamsha jamii juu ya athari za utawala mbaya na rushwa kwenye jamii.
“Nimechukua hatua kama waziri mwenye dhamana kuwaomba polisi kumuachia huyo kijana, wamuache kumuhoji na hata nitafurahi nikimuona kesho akija Dodoma ili nimshauri nini cha kufanya kwenye wimbo wake ili uwe mzuri zaidi,” alisema waziri Mwakyembe.
Waziri Mwakyembe ameongeza kuwa wao kama Serikali na wizara hawaoni madhara ya wimbo huo lakini akataka uboreshwe zaidi na kuwataja watu kama wakwepa kodi na wanaojihusisha na dawa za kulevya.

Post a Comment

 
Top