0

Wakati Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ikiwa imepitishwa, takwimu za Sauti za Wananchi na Afrobarometer zinaonyesha kuwa wananchi wanaunga mkono wajibu wa vyombo vya habari katika kuiwajibisha serikali

Kwa mujibu wa utafiti wa Afrobarometer, asilimia 65 ya wananchi wangependa vyombo vya habari vitoe taarifa za maovu yanayofanywa na serikali ikiwemo vitendo vya rushwa. Hata hivyo, asilimia 31 wanasema utoaji wa taarifa hizo utaiathiri nchi.

Ni wananchi 8 kati ya 10 (75%) wanaosema kuwa vyombo vya habari vinafanya kazi nzuri ya kufichua maovu na rushwa, huku wananchi 2 kati ya 10 (18%) wakisema havifanyi kazi nzuri. Kwa upande wa uhuru wa kutangaza habari, asilimia 53 wanasema vyombo vya habari viwe huru kutangaza habari yoyote huku asilimia 44 wakisema serikali iwe na mamlaka ya kufungia magazeti.

Vilevile, asilimia 65 wanasema vyombo vya habari havijawahi au kama vimeshawahi, ni mara chache sana vimekuwa vikitumia vibaya uhuru wake kwa kutangaza vitu ambavyo si vya kweli. Wananchi wanaunga mkono kwa kiasi kikubwa uhuru wa maoni na kupata taarifa. Karibu wananchi wote (95%) wanasema wananchi wawe huru kuikosoa serikali pale ambapo wanaona imekosea.


Pia wanaunga mkono demokrasia.  Takwimu za Sauti za Wananchi za hivi karibuni zinaonyesha asilimia 69 ya wananchi walichagua demokrasia kuliko aina nyingine ya serikali. Uungaji mkono huu wa demokrasia pia unadhihirika kupitia takwimu za Afrobarometer (2014) zinazoonesha asilimia 79 ya wananchi wakisema kuwa serikari inayoongoza kidemokrasia ndiyo aina ya serikali wanayoipenda zaidi na asilimia 81 wakisema ni vema wachague viongozi wao kupitia chaguzi huru za kidemokrasia.

Upatikanaji wa taarifa vilevile ni muhimu kwa wananchi. Asilimia 77 wanasema wananchi wa kawaida wawe na uwezo wa kupata taarifa zinazoshikiliwa na mamlaka za umma, huku asilimia 23 wakisema ni wale tu wanaofanya kazi kwenye mamlaka za umma ndiyo waruhusiwe kupata taarifa hizo.

Asilimia 80 wanasema upatikanaji wa taarifa hizo kwa wananchi utasaidia kupunguza vitendo vya rushwa huku asilimia 20 wakisema watumishi wa umma watatafuta njia nyingine za kuficha maovu yao.

Suala la kuunga mkono haki yao ya kupata taarifa za serikali, karibu wananchi wote (92%) wanasema ni muhimu kwa vipindi vya bunge kurushwa moja kwa moja kupitia luninga na redio. Asilimia 79 wanapinga maamuzi ya serikali ya kusitisha matangazo hayo na asilimia 88 wanasema bunge lirushwe moja kwa moja bila kujali gharama. Asilimia 12 wanasema wanadhani suala la kubana matumizi ni sababu nzuri ya kutokurusha vipindi ya bunge moja kwa moja.


Takwimu hizi zimekusanywa na Twaweza baada ya kutiwa saini kwa sheria mpya kandamizi ya Huduma za Vyombo vya Habari. Takwimu hizi ni za matokeo ya hivi karibuni ya utafiti wa Afrobarometer na Sauti za Wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza Aidan Eyakuze, anasema “Mwaka huu, 2016, umekuwa mwaka uliogubikwa na changamoto kwa haki za raia za kupata taarifa na kutoa maoni yao kwa uhuru. Matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kupitia luninga na redio yamesitishwa ndani ya mwaka huu japokuwa wananchi wengi wameendela kuomba yarejeshwe. Watanzania kadhaa wamechukuliwa hatua kali chini ya sheria ya Uhalifu wa mitandao kwa kosa la kutoa maoni yao, vile vile mwaka huu ndipo sheria kandamizi ya Huduma za Habari imepitishwa na Bunge na kutiwa saini na Rais. Takwimu zetu zinaonesha ya kwamba wananchi wanathamini sana nguzo kuu tatu za demokrasia imara; uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa maoni na haki ya kupata taarifa. Wananchi pia wana uelewa mpana juu ya madhara ya kuminywa kwa haki hizi muhimu kwa raia. Pia wanaelewa umuhimu wa kuwa na vyombo vya habari visivyokaliwa kooni. Ni vema maoni ya wananchi yaheshimiwe. Tunaamini kuwa busara, hekima, maamuzi sahihi yasiyo na upendeleo pamoja na fikra chanya vitaongoza utekelezaji wa sheria hii ya Huduma za vyombo vya habari."

Post a Comment

 
Top