Kwa mtu ambaye nilishiriki kikamilifu kufichua ufisadi wa ununuzi wa Airbus 320 kwa kushirikiana na wazalendo wengine naweza kusema kuwa kama tunafikiria kuwa ujio wa hizi ndege mpya utatatua tatizo la ATCL tutakuwa tumefanya makosa, au tutakuwa tumerudia makosa. Ikumbukwe kuwa ujio wa ile Airbus 320 nao ulifanywa kwa namna hii watu wakidhania kuwa kuja kwa ndege ile kungelifufua shirika.
Nina uhakika wengine wameonesha hili na mimi nalirudia tu kwa namna yangu; kwamba tatizo la msingi la kampuni hii - na inaweza taasisi na kampuni nyingine kadhaa serikali ambazo hazijafanya vizuri - kwa kiasi kikubwa ni tatizo la kiuongozi. Nyangenyange wanaporuka angani humfuata kiongozi wao; akiamua kuanza kutua na wao wanatua akiamua kwenda Magharibi na wao wanamfuata. Kanuni hii ipo katika viumbe vingi ambavyo huishi kwa kuwa na kiongozi; tembo, makundi ya simba, fisi hata baadhi ya wadudu huishi kwa kufuata viongozi wao; na wengine hufa wakimfuata kiongozi huyo.
Kampuni ya ATCL kwa muda mrefu imekuwa na shida hiyo ya uongozi; na hapa hatuzungumzii majina au mtu kuwa na qualifications za kisomi; tunazungumzia, maono ya kiuongozi, uthubutu wa maamuzi, usimamizi wa kiutawala, nidhamu ya kazi n.k Kiongozi akiwa dhaifu na akiwa ambaye hana maono yanayopasa ni vigumu sana kuweza kuongoza taasisi ambayo inataka kuingia kwenye ushindani ambapo wapo wengine wakifanya vizuri zaidi. Ni lazima kiongozi awe ni mtu ambaye ni trailblazer kweli kweli.
Tatizo hili la kiuongozi kwa kiasi kikubwa lilijionesha katika huduma. Na ninaamini kabisa, bila kuboresha huduma hata tuje na ndege zinazotumia warp engine bado tutajikuta tunakosa ushindani. Kama abiria - mteja - anapoanza kununua tiketi hadi hadi anashuka uwanjani hajihisi kuwa amepata huduma inayomstahili kutoka kwenye shirika lake ni vigumu sana kwa abiria huyo kurudi.
Tusije kutarajia watu wapande ndege za ATCL kwa ajili ya uzalendo; watu wanafuata huduma, unafuu wa bei, heshima na utu ambao unaonekana kuwepo. Nina uhakika tuna watu wanaoweza kutoa huduma ya kisasa, yenye heshima na yenye kuonesha kuwa wanajaliwa wateja kweli kweli. Hawa ndio watu wanaoweza kuvutia abiria kupanda ATCL. Ni lazima watu waone fahari kutumikia kampuni hii na wawafanye watu waone fahari kutumia kampuni hii.
Ni mpaka pale tutakapoweza kuwafanya watu waone kuwa hii ni kampuni ambayo ina new ethos na ina maadili ambayo yako juu ya kampuni nyingine yeyote ya ndege, basi uwezekano wa kufanikiwa kwa muda mfupi.
**from desk witter: M. M. Mwanakijiji
Post a Comment