DAR ES SALAAM.
Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita leo ameungana na wakazi wa jijini la Dar Es Salaam katika zoezi la kupima Magonjwa ya Kisukari na Presha lililoandaliwa na Lions Clubs International kwa kushirikiana na Kituo cha Afya cha Irania kilichopo jijini hapa.
PHOTO: Meya mwita (mwenye shati jeusi) akipimwa afya na Dokta Mahmod Shahamati (kulia) ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha Afya cha Iranian kilichopo Dar. |
Katika zoezi hilo Meya Mwita amewapongeza waandaaji na kuwaeleza kuwa wasiishie hapo bali wafikishe huduma hiyo kwenye halmashauri nyingine za jiji la Dar es Salaam ili wananchi wote waweze kupata huduma hiyo.
Mstahiki meya amesisitiza kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa wananchi kupima afya hususani inapojitokeza fursa hizo kwa kuwa baada ya kupata majibu ya vipimo hivyo inawapa urahisi katika kupata matibabu.
Ameongeza kuwa Taasisi hizo zimekuwa na mchango mathubuti kwa wananchi kutokana na uzalendo mkubwa waliokuwa nao na hivyo kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo.
"Jambo hili ni muhimu sana, ninawapongeza, ombilangu kwenu, angalieni namna ya kuendelea kuwasaidia wananchi wengine katika jiji letu la Dar es Salaam, huduma hii ni ya muhimu sana na kila mwananchi anahitaji kuipata" amesema Meya Mwita.
Awali akimkaribisha Meya Mwita, Rais wa Lions Clubs Shaheen Alam amempongeza na kumueleza kuwa wamekuwa wakitoa huduma hiyo kwa kushirikiana na Kituo cha Afya cha Iranian kwa lengo la kuwasaidia wananchi kutambua afya zao.
Post a Comment