0
PHOTO: IGP Simon Siro akiwa mjini Moshi. 

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro amesema mauaji ya polisi, viongozi na raia katika maeneo ya Kibiti, Rufiji na Ikwiriri ni ya muda na kusisitiza majibu yake yako mbioni kupatikana.


Sirro ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi) katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi (MPA), wakati wa kufunga mafunzo ya upandishaji vyeo kwa maofisa na askari 222 wa Jeshi la Uhamiaji nchini.

Kauli ya Sirro imekuja huku kukiwa na mfululizo wa mauaji ya polisi na raia katika maeneo hayo ambapo zaidi ya watu 35 wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakiwamo polisi 13.

Hadi sasa, licha ya polisi kufanya operesheni kubwa katika maeneo hayo, bado halijaweza kubaini chanzo cha mauaji hayo na kwa nini wanawalenga polisi na baadhi ya watu na nani wanayatekeleza.

Tukio la hivi karibuni kabisa lililotokea Jumatano iliyopita, ambapo watu wasiojulikana waliwashambulia kwa risasi na kuwaua polisi wawili wa kikosi cha usalama barabarani huko Kibiti.

Akizungumza katika sherehe za kuhitimu mafunzo kwa maofisa na askari hao 222 wa Jeshi la Uhamiaji, Sirro amesema japokuwa nchi ni salama, lakini inakabiliwa na kitisho cha usalama eneo hilo.

“Tuna shida Kibiti Ikwiriri lakini wanasema sisi ni wengi wao ni wachache. Tusikubali hata siku moja makabila yetu, madhehebu yetu, majimbo yetu yatugawanyishe,” amesema Sirro na kuongeza,

Umoja wetu ndio nguvu yetu. Suala la Kibiti ni la muda mfupi. Tunakwenda na tutapata majibu. Hatutakubali kikundi cha watu wachache wafanye Kibiti, Ikwiriri, Rufiji yasikalike,”.

Akizungumzia changamoto zinazolikabili Jeshi la Uhamiaji, Sirro aliyekuwa mgeni rasmi amesema moja ya changamoto kubwa ni uingiaji wa wahamiaji haramu wanaopitia njia zisizo rasmi kuingia nchini.

“Hili litawezekana kwa kuimarisha intelijensia. Mnapopanda vyeo sio mfurahie tu kupanda cheo mjue majukumu yanaongezeka pia. Idadi ya mnaoenda kuwaongoza sasa itaongezeka,”amesema Sirro.

PHOTO: IGP Siro (4th from left) Akikagua gwaride la askari wahitimu wa mafunzo. 


“Kazi yenu Uhamiaji na sisi polisi hazitofautiani sana na mara nyingi tumekuwa tukifanya kazi za operesheni pamoja. Changamoto tunayokutana nayo ni usimamizi wa kazi”alisisitiza na kuongeza;-

Askari anakosea huchukui hatua. Konstebo anafikia mahali anamtuma Koplo amletee soda na anakimbia anakwenda kumletea soda. Mnaona ni sawa hii?”alihoji na kujibiwa “Hapana”.


“Heshima yetu sisi askari ni kutokuwa waoga na unakuwa sio muoga kwa sababu kazi unaifahamu, unakuwa sio muoga kwa sababu unatii sheria na unasimamia sheria na hubabaiki,”amesema.

“Ninawaelekeza suala la uoga, suala la ulegelege katika awamu hii tusiipe nafasi,” ameongeza kusema na kusisitiza maofisa hao kufanya kazi kwa weledi pasipo kuwasumbua au kuwazungusha wananchi.

Kamishina Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji, Dk Anna Makakala, amesema mafunzo hayo ni ya kwanza katika historia ya jeshi lake baada ya Jeshi hilo kufanya maboresho ya kimuundo na sheria.

“Jeshi la Uhamiaji limefanya maboresho yakiwamo ya kimuundo na sheria ili kuliingiza Jeshi la Uhamiaji katika tume ya polisi na Magereza. Hatua hii imechangia kuwepo kwa mabadiliko,”amesema.

“Uhamiaji lina askari na watumishi wasiozidi 3,000, hawatoshi kutokana na ongezeko la majukumu ya uhamiaji. Ili kufanya kazi kwa ufanisi linalihitaji kuwa na askari wasiopungua 10,000,”amesisitiza.

Kamishina Jenerali hiyo amesema Taifa kwa sasa linakabiliwa na changamoto ya wahamiaji haramu wanaoingia kupitia njia zisizo rasmi, lakini akasema wanapata ushirikiano mkubwa toka polisi.

Post a Comment

 
Top